Wednesday, August 8, 2012

CAG Aanza Kuchunguza Madudu Tanesco

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema ofisi yake imeanza ukaguzi wa tuhuma zinazomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando.

Julai 14 mwaka huu, Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco ilimsimamisha kazi Mhando na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi wa Ununuzi, Harun Mattambo kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Utouh aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba ofisi yake imekabidhiwa kazi hiyo na tayari imeshaanza na imefikia pazuri. “Ni kweli suala hilo nimeshakabidhiwa na kazi hii tayari imeshaanza na imefikia pazuri. Kikao cha kwanza kimekaa Jumamosi iliyopita na mimi nimeshafika kuwahakiki maofisa wangu wanaoshughulikia hilo,” alisema Utouh na kuongeza kuwa kazi hiyo inaweza kukamilika ndani ya siku 60 kuanzia sasa.

Tuhuma zilizopo
Tuhuma za ufisadi Tanesco, zilianzia katika ripoti ya CAG ya mwaka huu ambayo ilionyesha gharama za ununuzi ziliongezeka kwa mwaka jana, kutoka Sh300 bilioni hadi 600 bilioni.
Baada ya sakata hilo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), ilitaka hatua zichukuliwe dhidi ya Bodi na Watendaji wa Tanesco na kuhoji ongezeko hilo kubwa la gharama za ununuzi.

Lakini wiki mbili kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, bodi hiyo iliitisha kikao cha dharura Julai 13, mwaka huu kujadili tuhuma mbalimbali dhidi ya menejimenti ya shirika hilo na kuamua kwamba tuhuma dhidi ya Mhando ni nzito hivyo ni vyema zifanyiwe uchunguzi huru na wa kina.

“Hivyo, Bodi iliazimia pamoja na mambo mengine kama ifuatavyo: Uchunguzi wa tuhuma hizo uanze mara moja kwa kutumia uchunguzi huru na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando ili kupisha uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini.”
“Pamoja na uamuzi huo, Bodi imechukua hatua stahiki za kuhakikisha kwamba shughuli za utendaji na uendeshaji wa Tanesco zinaendelea kama kawaida,” ilisema taarifa hiyo.

Sakata hilo lilipamba moto bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kwa 2012/13. Akiwasilisha Bajeti hiyo, waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo alisema mbali ya tuhuma za kupanga mgawo wa umeme kama mkakati na kampuni za mafuta, Mhando pia anadaiwa kuidhinisha zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi kwa kampuni ya mkewe, Eva Mhando. Profesa Muhongo alisema zabuni hiyo ni zaidi ya Sh800 milioni na kwamba, Eva alitumia kampuni ya Santa Clara na Mhando aliidhinisha pasipo kutangaza mgongano wa kimasilahi. Tuhuma hizo na nyingine zilihusisha baadhi ya wabunge na kumfanya Spika, Anne Makinda kuivunja Kamati ya Nishati na Madini baada ya kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz

No comments: