Tuesday, August 7, 2012

Madaktari Kujadili Hali Ya Dr Ulimboka

WAKATI kukiwa na taarifa za kurejea nchini kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka viongozi wa Jumuiya hiyo na Umoja wa Madaktari Tanzania (MAT), wanatarajia kukutana leo kujadili mkanda mzima wa sakata lililomkumba kiongozi huyo.  Baada ya kikao hicho, madaktari hao watakutana na familia yake na kisha kumuuliza Dk Ulimboka kama angependa kilichomtokea kiwekwe wazi kwa jamii.

 Dk Ulimboka ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea nchi nzima, alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatato ya Juni 27 mwaka huu na kupelekwa katika msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji a Dar es Salaam, ambako aliteswa na kujeruhiwa vibaya.

Katika tukio hilo daktari huyo aling’olewa meno mawili na kucha za mkono mmoja na baadaye kulazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalum (ICU) katika Taasisi ya Mifupa (MOI).  Baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya Juni 30 mwaka huu, alisafirishwa kwenda Afrika a Kusini kwa ajili ya vipimo na matibabu.

 Kusafirishwa kwake kulifuatia taarifa ya jopo la madaktari lililokuwa linamhudumia kutoa taarifa kwa madaktari bingwa kuhusu abadiliko ya afya.

 Taarifa za kurejea kwa Dk Ulimboka zimezagaa katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam, huku baadhi ya watu wakizijadili katika mitandao ya kijamii.  Akizungumza na gazeti hili Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Edwin Chitage, alisema kuwa hali ya Dk Ulimboka inazidi kuimarika lakini alisita kueleza wazi ni lini kiongozi huyo wa madaktari atarudi nchini.

 “Tukiwa tayari tutatoa taarifa katika vyombo vya habari juu ya suala zima la afya ya Dk Ulimboka,” alisema Dk Chitage.  Alisema leo au kesho viongozi mbalimbali wa MAT na Jumuiya ya Madaktari, watakutana kujadili suala la kiongozi huyo.

 “Ndani ya siku mbili hizi (leo na kesho) viongozi tutakutana na kujadili ripoti ya matibabu ya Dk Ulimboka na tutajadili kama tuvieleze vyombo vya habari ama laa,” alisema Dk Chitange.  Hata hivyo Dk Chitange alisema hatua hiyo itategemea na kauli ya familia ya Dk Ulimboka na  yeye mwenyewe (Dk ULimboka) kwa kuwa na wao pia watashirikishwa.

 “Dk Ulimboka na familia yake tutawashirikisha katika mambo ambayo tutayajadili,” alisema Dk Chitage. 

    Alipoulizwa kama kiongozi huyo wa madaktari sasa anaweza kufanya shughuli zake kama awali, alisema hana uhakika kwa kuwa hana taarifa za ndani zaidi . CHANZO: MWANANCHI

No comments: