Saturday, March 16, 2013

Uchaguzi wa Kamati za Bunge:Vita Lowassa,Membe yakolezwa

                                              Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa

Dar es Salaam. Ofisi ya Bunge jana ilitangaza majina ya wenyeviti na makamu wapya wa Kamati za Kudumu za Bunge huku Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Kuchaguliwa kwa Lowassa kuongoza kamati hiyo kunaibua upya vita kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kutokana na wote kutajwa kutaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015. Awali

, Lowassa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ambayo iligawanywa hivi karibuni na kuzaliwa kamati mbili; ya Ulinzi na Usalama na Kamati ya Mambo ya Nje. Kushinda kwa Lowassa kunakuja siku moja, baada ya wabunge wote wa CCM kukutana katika kikao cha ndani kilichofanyika Ukumbi wa Karimjee na kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuwachagua wenyeviti na makamu wa kamati hizo.

Habari za ndani kutoka katika kikao hicho zilieleza kuwa moja ya ajenda zilizozungumzwa ni kuwataka wabunge kuwachagua wenyeviti kwa kufuata taratibu na utendaji wao wa kazi.

Hata hivyo, Naibu Spika Job Ndugai aliliambia Mwananchi Jumamosi kwamba kikao hicho ni cha kawaida na walikuwa wakijadiliana matatizo yaliyopo katika majimbo yao na jinsi ya kuyawasilisha serikalini.

Katika uchaguzi huo, Musa Azzan Zungu ambaye alikuwa makamu wa Lowassa kabla ya kugawanya kwa kamati hiyo, amechaguliwa tena kushika nafasi hiyo.

Uchaguzi wa wenyeviti na makamu wao ulifanyika jana katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada ya ofisi ya Bunge kutaja majina ya kamati mpya 16 pamoja na wajumbe wake.

Uchaguzi huo umefanyika ukiwa umepita mwezi mmoja tangu kumalizika kwa mkutano wa 10 wa Bunge ambapo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).

Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo wakati zimeundwa kamati mpya za Bajeti, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ya Ulinzi na Usalama.

Taarifa za ndani kutoka katika chaguzi hizo zinaeleza kuwa Zitto ambaye alikuwa akichuana na John Cheyo, alipata kura 13 kati ya 17 zilizopigwa na wajumbe wa kamati yake, hivyo Zitto sasa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).

No comments: