Tuesday, January 8, 2013

WASTARA; MKE MWEMA ALIYEPIGANIA ROHO YA MUMEWE HADI DAKIKA ZA MWISHO

     Siku ambayo wapendanao hao walifunga ndoa  lakini wastara akawa na kilio cha kupoteza mguu


                                         Siku ambayo walisimamia harusi ya msanii mwenzao
SAFU ya Kali Wiki hii inakuja na tukio lililotikisa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam ambapo tasnia ya filamu kwa mara nyingine ilimpoteza muigizaji wake maarufu, Juma Kilowoko almaarufu kama Sajuki.

Kifo cha Sajuki ni pigo katika tasnia hiyo lakini zaidi kwa mkewe, Wastara Juma ambaye alifanya kila juhudi kupigania uhai wa mumewe hadi dakika za mwisho lakini Mungu akampenda zaidi na kumchukua Januari 2, mwaka huu akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa kwa matibabu.
Hatuwezi kusema mengi sana kuhusu kifo hicho kwani mnajimu maarufu nchini, marehemu Sheikh Yahya Hussein aliwahi kusema kwamba kupinga kifo ni kumkufuru Mungu kwa sababu hiyo ni amri yake.

Lakini ukweli unabaki palepale kwamba Sajuki na Wastara walikuwa ni wanandoa waliopendana sana katika maisha ya ndoa yao ambayo ni mafupi sana kwani walioona Juni 6, 2009 na baada ya hapo mikosi kedekede ikawa inawaandama.
Mateso ndani ya ndoa yao yalikuwa kama ni kupokezana kijiti na kuwafanya kutokwa na machozi ya huzuni. Sajuki ameugua kwa muda mrefu maradhi ya uvimbe tumboni ndiyo chanzo cha matatizo yake yote.

Katika maisha yao ya ndoa, wawili hao wamekuwa wakipokezana mateso huku likiibuka jipya la kuwatoa machozi mara kwa mara na sasa Sajuki ndiye anayewaliza watu kufuatia kusumbuliwa na maradhi ya uvimbe tumboni.

Leo tuwape historia fupi ya maisha yao ya mashaka na huzuni tukianzia Machi 12, 2009 wakati huo wakiwa wachumba tu,  Wastara na Sajuki walipata ajali mbaya ya pikipiki maeneo ya karibu wanapoishi, Tabata, Dar es Salaam ambapo mwanadada huyo alikatika mguu, hapo ndipo huzuni ya wapendanao hao ilipoanza kuwafuata. Walisikitishwa sana na tukio hilo baya katika maisha yao.
Wapendanao hao walifunga ndoa  lakini Wastara akawa na kilio cha kupoteza mguu na kutaka wa bandia ambao ulikuwa na gharama kubwa. Mungu si Athmani kwani walifanikiwa kupata shilingi milioni 7 zilizomfanya mwana mama huyo kwenda Nairobi Kenya na kupata

Historia ya maisha yao inaonesha kuwa Agosti 29, mwaka juzi Wastara alikimbizwa hospitalini na kulazwa kutokana na maradhi ya nimonia ambayo yalimjia ghafla. Lakini uchunguzi ulipofanywa alionekana pia kuwa alikuwa mjamzito, japokuwa mwenyewe alifanya siri.

Habari kwamba Sajuki ni mgonjwa zilivuma Oktoba 29, mwaka 2011 na ikagundulika kuwa alikuwa na uvimbe tumboni na saratani ya ngozi. Baya zaidi gharama za tiba zilikuwa kubwa kwani zilikuwa zikihitajika shilingi milioni sita, na wao kwa kuwa walikuwa hawana, furaha ya maisha ikadidimia
Lakini Mungu naye ana mambo yake kwani Machi 7, mwaka jana wakati fedha za matibabu India zikiwa zimepatikana kwa michango mbalimbal ndoa yao ilipata Baraka za Mungu kwa kupata mtoto. Ni bahati mbaya kwamba furaha yao haikukamilika kutokana na Sajuki kuugua.

Sajuki alifanikiwa kwenda India kutibiwa na Aprili 2, 2012 akarejea nchini kutoka katika Hospitali ya Apollo alikopelekwa kupata matibabu ambapo alisema alikuwa amepata nafuu kidogo kabla ya hivi karibuni hali kuwa mbaya zaidi na kuibua vilio upya kutoka kwa marafiki zake na hasa mkewe Wastara.
Zilisambazwa habari kwa Watanzania kuombwa kumchangia ili arudishwe India kwa matibabu lakini kabla ya mipango hiyo kukamilika Mungu akamchukua alfajiri ya Januari 2, mwaka huu na akazikwa Ijumaa iliyopita katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, mazishi ambayo yaliongozwa na Rais Jakaya Kiwete. Hakika Wastara alipigania roho ya mumewe kwa nguvu zake zote na ameonyesha upendo wa hali ya juu, anafaa kuigwa na wanandoa wengine!


No comments: