Thursday, March 7, 2013

TFF YASALIMU AMRI YA SERIKALI...UCHAGUZI UTARUDIWA UPYA

Serikali imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuandaa upya mchakato wa uchaguzi wake mkuu uliolalamikiwa na wadau mbalimbali wa soka nchini, kiasi cha wengine kufungua kesi mahakamani kuupinga.

TFF imeshitakiwa mahakama za Mwanza na Tanga, baada ya baadhi waliokuwa wagombea wa nafasi mbalimba kuenguliwa kwenda kortini kupinga kufanyika uchaguzi huo mpaka kesi zao za msingi zitakaposilizwa.

Kabla ya mchakato huo, TFF pia imetakiwa kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya katiba kabla ya Aprili 15, na baada ya hapo kuitisha pia Mkutano wa Uchaguzi kabla ya Mei 25 mwaka huu.

Uamuzi huo wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ulifikiwa jana katika kikao cha pamoja kati ya waziri mwenye dhamana ya kusimamia michezo, Fenella Mukangara na uongozi wa juu wa TFF.

Mwanzoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema wamewasilisha barua kwa Waziri Mukangara kutaka kukutana naye Alhamisi (leo) na kama ikishindikana wakutane baada ya March 13.

Osiah alisema katika kikao hicho, walipanga kukutana na waziri peke yake bila Naibu Waziri Amos Makala. Kwa siku za karibuni, Makala na Osiah wamejikuta kwenye mjadala mkali wa kurushiana maneno.

Hata hivyo, habari za ndani kutoka wizarani zinadai kuwa, Mkangalla amekataa ombi la awali TFF kukutana naye leo au Machi 23, na badala yake aliwataka viongozi wa TFF kukutana nao jana.

Kikao hicho mbali na waziri na naibu wake, pia alikuwamo Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi na Katibu wake Henry Lihaya, wakati TFF; Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni na mwanasheria wa TFF aliyewakilisha Kamati ya Utendaji, Alex Mgongolwa.

"Mchakato wa uchaguzi unaanza upya, wameambiwa waitishe mkutano mkuu wa marekebisho ya katiba na kuingiza marekebisho yote kuanzia ya mwaka 2007 hadi 2010 kwa kuwa katiba iliyopo kwa Waziri ni ile ya mwaka 2006.

TFF wametakiwa ndani ya siku tano kuanzia leo (jana) mpaka Machi 11 (Jumatatu) kutoa tamko la kukubali kutekeleza agizo la Serikali," kilisema chanzo cha habari ndani ya wizara.

Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa vile hajapewa barua ya maelekezo kutoka serikali, ingawa habari zilizopatikana baadaye barua hiyo imeshatumwa TFF.

Uchaguzi wa TFF uliingia dosari baada ya baadhi ya wagombea kuenguliwa kwa sababu mbalimbali, hiku wengine wakipeleka malalamiko Shirikisho la Soka Ulimwenguni (Fifa), ambalo linatarajia kutuma wawakilishi wake kuja kutatua mzozo huo.

No comments: