Thursday, January 31, 2013

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MWANGOSI NA ASKARI WENZAKE WAMDHARAU HAKIMU, WAOMBA MSAMAHA‏



 Askari  polisi wakimrejesha mahakamani mtuhumiwa  wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa  wa Iringa Daudi Mwangosi, askari  wa FFU mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (aliyevaa kofia nyekundu)  baaada ya kutoroshwa  kizimbani kabla ya mahakama kumaliza shughuli zake jana.


                                  Pasificus Cleophace Simoni akirudishwa ndani ya mahakama.
SAKATA la mtuhumiwa wa mauaji ya  aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa marehemu Daudi Mwangosi limezidi kuchukua  sura  mpya baada ya askari waliomfikisha mtuhumiwa  huyo wa mauaji  askari  wa FFU mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (23) kumtibua hakimu na kuagiza mtuhumiwa huyo kurudishwa tena kizimbani kwa kudharau mahakama hiyo.

Tukio  hilo lilitokea jana majira ya saa 5.35 asubuhi kwa askari  hao watatu ambao majina yao hayakuweza kufahamika mara moja  kumshusha  kizimbani mtuhumiwa  huyo wa mauaji na kumkimbizia mahabusu kama njia ya kukwepa kupigwa picha na wanahabari  waliokuwepo hapo lilitokea mara baada ya mahakama hiyo kuombwa kutaja tarehe nyingine ya  kutajwa kesi hiyo.

Huku  bado mahakama ikiwa inaendelea kwa hakimu kutaja tarehe ya kesi hiyo ya mauaji namba 1 ya mwaka 2012 mtuhumiwa huyo alishuka kizimbani akiwa kavaa kofia ya sweta (mzula) na miwani ya nyeusi na kuanza kuondoka.

Wakati hakimu akijiandaa kusimama ili kuhitimisha shughuli za kimahakama kwa siku  hiyo ghafla alijikuta anabaki na mwanasheria  wa mahakama, kalani wake, wanahabari, askari mmoja na ndugu  wawili wa mtuhumiwa huyo  huku askari  watatu wenye silaha  na mtuhumiwa huyo  wakiwa tayari wameondoka ndani ya chumba cha mahakama.

“Mbona hao askari wanamtoa mtuhumiwa  bila utaratibu wa mahakama? hebu  mwanasheria waambie wamrudishe ndani mtuhumiwa ....huu si utaratibu mbona  wanafanya fujo mahakamani  hao?” alisikika akisema hakimu mkazi  wilaya ya Iringa, Dyness Lyimo.

Hata  hivyo pamoja na jitihada za mwanasheria  wa  serikali, Adolf Maganda kuwaita  kwa  sauti  askari hao  kuwataka  kumrudisha  ndani ya mahakama mtuhumiwa huyo, bado askari walizidi kukimbia na mtuhumiwa kwenda nae mahabusu na baada ya dakika kama 5 hivi ndipo mwanasheria  huyo aliporejea na askari hao na mtuhumiwa ambaye hata  hivyo hakwenda kusimama  kizimbani na badala  yake alikwenda upande wa  kushoto wa mahakama  hiyo ambako alikuwa amekaa mwanzoni kabla ya mahakama  kuanza na kuketi katika  kiti huku akiwa amevaa miwani na kofia  yake.

Kutokana na  tukio  hilo hakimu alilazimika  kuwahoji askari hao  watatu kwa vurugu  hizo  walizozifanya kwa kuwauliza swali moja  pekee  kuwa  wanaona walichofanya ni  sahihi na askari hao kuomba msahama.

Mwendesha mashtaka  wa jamhuri, Adolf Maganda aliiomba mahakama hiyo kutaja tarehe nyingine ya kutajwa tena  kesi hiyo ambayo ilitajwa Januari 27 na mtuhumiwa huyo kushindwa kufika kutokana na tatizo la ugonjwa  lililokuwa likimsumbua.

Hata  hivyo mahakama  hiyo  iliahirisha  kesi hiyo  hadi  Februari 14 mwaka huu kesi hiyo itakapofikishwa mahakamani hapo kwa  kutajwa tena.

Mtuhumiwa  huyo anatuhumiwa  kumuua kwa makusudi kwa bomu aliyekuwa  mwandishi  wa habari wa Channel Tena  mkoa  wa Iringa marehemu Mwangosi  Septemba 2 mwaka jana  katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa  wakati  wa vurugu kati ya  polisi na wafuasi wa  Chadema kinyume na kifungu cha sheria namba 148 kifungu kidogo 5A.i cha makosa ya jinai. Kwa mujibu wa kesi za jinai, sheria kifungu 196 kanuni ya adhabu Cap. 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

(Picha na Francis Godwin)
Na Francis Godwin, Iringa

No comments: