Saturday, April 13, 2013

NAULI MPYA NCHINI SASA NI VURUGU TUPU

Viwango vipya vya nauli za daladala na mabasi yaendayo mikoani zimeanza kutumika jana, huku wananchi wakizipinga wakidai zinawaumiza zaidi kiuchumi.

Wakati baadhi wakilalamikia kupanda kwa nauli za dalala katika maeneo yao, baadhi ya wafanyakazi wa mabasi yaendayo mikoani wameendelea kutoza nauli ya zamani.

Zoezi la kupandisha nauli nchini lililoanza jana limewagawanya wamiliki wa magari na kufanya baadhi ya safari za mikoani kupandisha nauli, huku nyingine zikiendelea kuwa kama zamani wakati nauli za daladala Dar es salaam zikipanda kama ilivyoagizwa.

Hatua hiyo ya kupandisha nauli ilizua tafrani baina ya makondakta na abiria waliokuwa wakisafiri katika safari mbalimbali ndani ya jiji, hususan wale waliokuwa hawajui kuwa jana ndiyo siku ambapo nauli zilitakiwa kupanda.


Mwananchi liliweka kambi katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendeyo mikoani cha Ubungo tangu saa 12 asubuhi na kushuhudia baadhi ya abiria wa safari za Arusha na Kilimanjaro wakibishia kiwango cha juu cha nauli kilichopanda, hali iliyowafanya baadhi ya abiria kutishia kususia safari.

Hata hivyo, walilazimika kulipia kiwango hicho cha ziada kutokana na umuhimu wa safari zao japo kwa majibizano na mawakala wa kukatisha tiketi waliopo kituoni hapo.

Kwa mujibu wa Ofisa wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), Gervas Rutaguzinda safari za mikoani ambazo zilipandisha bei ya nauli ni Arusha, Moshi, Mwanza, Bukoba, Musoma na Kigoma huku nyingine zikiendelea kama zamani.
Alisema awali nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha kwa basi la kawaida ilikuwa Sh18,900 lakini jana tiketi zilikuwa zikiuzwa kwa Sh22,700 ambapo kutokana na ugumu wa kupatikana chenji abiria walitakiwa kulipa Sh23000.

“Nimewapokea watu watano wa kwenda Mwanza na wawili wa safari ya Kigoma ambao walileta malalamiko kuwa walishindwa kusafiri kutokana na kukosa ongezeko la nauli walilokutana nalo” alisema Rutaguzinda.

Alisema baadhi ya wamiliki wa basi walibainisha kuwa watapandisha nauli ifikapo mwezi wa sita, lakini kwa sasa wataendelea na nauli zao za kawaida.

Naye wakala wa kukatisha tiketi kwa safari za Arusha na Moshi aliyejitambulisha kwa jina moja la Ipiana alisema ongezeko hilo limeathiri pato lao kwa kuwa katika nauli ya awali alikuwa akipata Sh2,000 kama kamisheni kwa kila tiketi, lakini kwa jana fedha zote zlitakiwa kupelekwa kwa mmliki wa basi.

No comments: