Saturday, July 7, 2012

Barabara za Kupunguza Msongamano na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi

                                       Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Jana usiku tarehe 6 Julai 2012 Bunge limepitisha mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2012/2012. Mtakuwa mmeona wakati bunge lilipokaa kama kamati nilishika mshahara wa Waziri kutaka maelezo ya kisera juu ya mkakati wa serikali katika kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika barabara ya Morogoro inayopita Jimbo la Ubungo.
Nilitaka maelezo hayo kwa kuwa pamoja na kuunga mkono uwekezaji kwenye upanuzi wa barabara kuu, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa fly overs, miradi hii kwa ujumla wake inachukua muda wa kati na muda mrefu hivyo kukamilika kwake ni mpaka mwaka 2016 au zaidi.
Nilitaka maelezo ni kwanini Serikali isizingatie vipaumbele vya mwaka wa kwanza wa mpango wa miaka mitano katika kuandaa bajeti ili pamoja na miradi hiyo niliyoitaja iwekeze kwa haraka kwenye barabara za pete/mzunguko (ring roads) za pembezoni ambazo zinaweza kujengwa kwa kiwango cha lami katika kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuchangia kwenye kupunguza foleni katika barabara kuu ifikapo mwaka 2013.


Kufuatia majibu ya Waziri nilihoji tena wakati bunge linapitisha vifungu vya miradi ya maendeleo kwenye kasma ya kuondoa foleni Dar e salaam ambayo imetengewa shilingi bilioni 10.5 tu, wakati ambapo mpango wa taifa wa miaka mitano uliopitishwa umeelekeza kifungu hicho kitengewe jumla ya fedha kwa miaka miwili 2011/2012 na 2012/2013 kiasi cha shilingi bilioni 100.1 Ikumbukwe kwamba mwaka jana serikali ilitenga bilioni 5 tu wakati mpango uliitaka serikali itenge bilioni 68 na nilipohoji wakati huo nilijibiwa kwamba ilikuwa ni kipindi cha mpito hivyo fedha zote zingeunganishwa mwaka huu kitu ambacho hakikufanyika.

Majibu ya kwamba Dar es salaam na Pwani kwa ujumla zimetengewa bilioni zaidi ya 900 yanajumuisha fedha za maendeleo kwa miradi iliyoanza 2010/2011, 2011/2012, 2012/2013 na ni miradi ya muda mrefu ya barabara kuu na madaraja makubwa kwa mikoa yote miwili.

Kwa hiyo bilioni 10.5 imegawanywa kidogo kidogo kwa barabara zifuatazo: Mbezi Luis kupitia Goba mpaka Mbezi Tangi Bovu; Mbezi kwa Yusuph- Msakuzi- Mpiji Magohe mpaka Tegeta/Bunju; Mbezi-Malambamawili-Kinyerezi, Kimara-Mavurunza-Bonyokwa; Kimara-Kilungule-Makoka-Makuburi, Kimara-Matosa-Mbezi; Ubungo-Msewe-Chuo Kikuu na nyingine katika maeneo mengine ya Dar es salaam kama zilivyoelezwa katika hotuba ya Waziri. Kwa kasi hii ndogo, itachukua takribani miaka kumi kuweza kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hizo ambazo jumla ya urefu wake ni kilomita 96 tu.

Nashukuru kwamba fedha zimetengwa kumalizia pia barabara ya Ubungo Maziwa- Bus Terminal na pia za kuanza ya kuelekea External, na pia bilioni zaidi ya 240 za mradi wa DART; hata hivyo, tuendelee kuungana katika kuisimamia serikali ili itenge bilioni 100 kujenga kwa kiwango cha lami barabara tajwa za pembezoni za kupunguza msongamano haraka zaidi wakati tukisubiri utekelezaji wa miradi ya muda wa kati na muda mrefu.

Tuendelee kuishauri Tume ya Mipango ambayo Mwenyekiti wake ni Rais kuingiza kwenye Mpango wa Mwaka wa Maendeleo Mwezi Februari 2013 ili hatimaye kiwango hicho cha fedha kiingizwe katika bajeti. Izingatiwe pia kuwa sehemu ya Barabara hizo ni ahadi za Rais alipotembelea Jimbo la Ubungo kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010 na kurudia tena ahadi hizo wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2010. Tuendelee kushirikiana katika kufuatilia kazi za maendeleo.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
7/7/2012-Bungeni, Dodoma

http://mnyika.blogspot.com

No comments: