Tuesday, July 31, 2012

KAULI ZA BAADHI YA WABUNGE KUHUSU RUSHWA BUNGENI.

Baada ya kuwepo malalamiko ya rushwa kutembea bungeni na kusababisha kuvunjwa kwa kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya Wabunge wametaka majina ya wenzao wanaojihusisha na rushwa yawekwe wazi na wafukuzwe bungeni.

Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari (CHADEMA) amesema pamoja na kwamba kamati ya nishati na madini imetajwa moja kwa moja, zipo kamati nyingine ambazo wabunge wake wanatajwa kuhusika na kuomba rushwa.

Amesema “zipo kamati kadhaa zinatuhumiwa kwa rushwa, Mh Spika nilikua naomba muongozo wako kwamba kwa nini ofisi yako isiamue kuzivuruga kamati kadhaa ambazo zinatuhumiwa kwa rushwa ikiwemo kamati ya kudumu ya bunge ya Serikali za mitaa inayoongozwa na Mh. Mrema na Kamati ya kudumu ya bunge ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mh. Zitto Kabwe, hii ni kwa sababu wabunge wengi wamekua wanazikimbilia zile kamati ambazo zina mikataba lakini kamati kama ya maendeleo ya jamii ya huduma za jamii ambazo zina umuhimu mkubwa kwenye nchi kwa sababu hazina mikataba zinakimbiwa”

Mbunge wa Lindi mjini Salum Khalfan na mbunge wa Nkasi kaskazini Ally keissy Mohamed wamelitaka bunge kuwafukuza bungeni wabunge wote watakaogundulika kula rushwa, wanataka watajwe kwa sababu sasa hivi wabunge wengine kila wakipita barabarani wanakosa raha kutokana na hiyo kashfa ya rushwa iliyolichafua bunge.

Baada ya hayo Naibu Spika wa bunge Job Ndugai aliomba kamati ya uongozi wenyeviti wa kamati za bunge kukutana na Spika kulizungumza ili baadae wampe maelekezo zaidi.

No comments: